25 KCCO ANIVERSARY
Leo, Kilimanjaro Centre for Community Opthalmology (KCCO) imeandika historia kwa kuadhimisha miaka 25 ya huduma, ubunifu na mchango mkubwa katika kuzuia upofu na kuboresha huduma za afya ya macho nchini Tanzania na kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gileard Masenga, alitoa pongezi kwa KCCO kwa safari yake ya robo karne iliyojengwa katika misingi ya kujitolea, ubora wa huduma, elimu, tafiti na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa afya ya macho. Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa mafanikio ya KCCO hayaonekani tu katika idadi ya miaka iliyopita, bali yanaakisiwa katika maelfu ya maisha ya watu yaliyoguswa na kubadilishwa kupitia upatikanaji wa huduma bora za macho, mafunzo ya wataalamu, tafiti na huduma za kijamii.
Prof. Masenga alieleza kuwa KCMC itaendelea kuimarisha ushirikiano na KCCO pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora za afya ya macho. Aidha, alitoa shukrani za dhati kwa washirika wote waliounga mkono KCCO kwa kipindi cha miaka 25, akiwemo CBM na wadau wengine, ambao mchango wao umewezesha kuboresha maisha ya watu wengi kupitia huduma za macho.
`Maadhimisho haya yamekuwa fursa ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana, kuthamini ushirikiano uliopo, na kuweka upya dhamira ya kuendeleza tafiti, ubunifu, matumizi ya teknolojia za kidijitali, mafunzo ya wataalamu na utoaji wa huduma za afya ya macho kwa jamii ili kuondoa upofu unaoweza kuzuilika na kuboresha ubora wa maisha ya wananchi`. alisema Prof. Masenga
Hongera KCCO kwa miaka 25 ya mafanikio. Tuendelee kushirikiana kujenga jamii yenye afya bora ya macho kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Related Stories