MASHUJAA WA SARATANI MTAMBUKA WAKUTANA KCMC
Moshi, Kilimanjaro | 28 Julai 2027
Shirika la Aga Khan Foundation Tanzania, kupitia mradi wa East Africa Comprehensive Women Cancer Project (EACWCP), kwa kushirikiana na Shujaa Cancer Foundation, leo limeendesha warsha katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini - KCMC kwa lengo la kuwatambua na kuwahamasisha manusura wa saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi kuunda kikundi rasmi cha Mashujaa wa Saratani Mtambuka.
Warsha hiyo imelenga kuwajengea uwezo washiriki ili wawe mabalozi wa afya katika jamii kwa kutoa elimu kuhusu kinga, dalili na umuhimu wa uchunguzi wa mapema wa saratani. Aidha, kikundi hicho kitahamasisha wanawake kujitokeza kupata huduma za uchunguzi na matibabu kwa wakati, pamoja na kutoa msaada wa kihisia na kushirikiana uzoefu wao na wagonjwa pamoja na manusura wenzao. Juhudi hizi zinatarajiwa kuongeza uelewa wa jamii, kupunguza unyanyapaa unaohusishwa na saratani, na kuchangia kupunguza vifo vinavyotokana na saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Mkurugenzi wa Shujaa Cancer Foundation, Bi. Gloria Kida, alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa kikundi hicho, akieleza kuwa kitakuwa jukwaa muhimu kwa manusura wa saratani kuelimisha jamii, kuhamasisha uchunguzi wa mapema na kutoa matumaini kwa wagonjwa wengine kupitia ushuhuda na uzoefu wao.
Kwa upande wake, Afisa Mradi wa Aga Khan Foundation Tanzania, Gega Bujeje, aliwahimiza mashujaa hao kulitumia jukwaa hilo kuwa chanzo cha faraja, matumaini na hamasa kwa wagonjwa wa saratani. Alieleza kuwa Aga Khan Foundation itaendelea kushirikiana nao na kuwaunga mkono katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zitakazochangia kuboresha afya na ustawi wa wanawake katika jamii.
Related Stories