2026-02-11 00:00:00
β’
DAMU
β’
5 min read
ALFA WANAVYOKUSANYA DAMU KWA NAMNA NYINGINE
Kikundi cha Alfa Victory Women Group kutoka Njiro, Arusha, kikiongozwa na Mwenyekiti wao Bi. Inviolata Mushi, kimetembelea Hospitali ya KCMC kwa lengo la kutoa mchango maalum utakaowezesha KCMC kuendelea na zoezi la ukusanyaji wa damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma za dharura.
Ziara hiyo imefanyika kwa dhamira ya kuunga mkono juhudi za KCMC katika kuhakikisha upatikanaji wa damu salama kwa wagonjwa. Kwa sasa, KCMC ina mahitaji makubwa ya damu ambapo hutumia wastani wa paketi 50 hadi 60 za damu kwa siku kwa ajili ya wagonjwa wanaopata matibabu mbalimbali ikiwemo akina mama wajawazito, watoto wachanga, wagonjwa wa ajali pamoja na wanaofanyiwa upasuaji.
Akizungumza wakati wa kupokea mchango huo, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara KCMC, Prof. Ireen Kiwelu, aliwashukuru wanakikundi cha Alfa Victory Women Group kwa moyo wao wa kujitolea waliouonesha kwa vitendo. Prof. Kiwelu amesema mchango huo utaiwezesha KCMC kufika katika jamii na kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la utoaji damu ili kuongeza akiba ya damu salama kwa matumizi ya hospitali.
βMahitaji ya damu KCMC ni makubwa kila siku, hivyo msaada wenu ni wa thamani sana. Utawezesha kufika kwenye jamii na kuwahamasisha wananchi kutoa damu kwa hiari kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine,β alisema Prof. Kiwelu.
Aidha, Prof. Kiwelu aliahidi kuunga mkono juhudi zilizooneshwa na kikundi hicho kwa kuhamasisha pia vikundi vingine alivyokuwa navyo kushiriki katika kampeni za utoaji damu, akisisitiza kuwa ni jambo la baraka, lenye manufaa kwa jamii na linalopendeza machoni pa Mungu.
Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Hagai Chapel β KCMC, Mch. Neema Ndoki, alibariki mchango uliotolewa na Alfa Victory Women Group na kuwaombea wanakikundi hao waendelee kuwa na moyo wa upendo na kusaidia wahitaji katika jamii.
Related News