RADIOLOJIA YASONGA MBELE
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini - KCMC kwa kushirikiana na @radaidinternational pamoja na Chuo Kikuu cha Chicago, leo imezindua rasmi mafunzo maalum ya siku mbili yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma za radiolojia.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gileard Masenga alieleza kua hii ni hatua ya kihistoria katika safari ya hospitali kufikia viwango vya kimataifa katika huduma za uchunguzi wa magonjwa kupitia teknolojia ya picha za mwili (body imaging). Alisisitiza kuwa ushirikiano huu wa kimataifa unaenda mbali zaidi ya mafunzo ya kawaida, kwani unajenga daraja la maarifa, ubunifu na uzoefu kati ya wataalamu wa ndani na wenzao wa kimataifa.
Katika hotuba yake, Prof. Masenga alibainisha kuwa KCMC imejipanga kuhakikisha kuwa kila mtaalamu iwe ni daktari bingwa wa radiolojia, daktari wa tiba, muuguzi au mtumishi msaidizi anakuwa sehemu ya mabadiliko haya, kwa kutambua kuwa huduma bora za radiolojia ni msingi muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kitabibu.
Mafunzo haya yanatoa jukwaa adhimu la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kisasa zaidi katika sekta ya radiolojia, yakihusisha matumizi ya teknolojia ya hali ya juu pamoja na uelewa mpana wa namna taswira za mwili zinavyoweza kusaidia katika kupanga matibabu ya upasuaji na tiba nyinginezo. Aidha, ushiriki wa wataalamu kutoka kada mbalimbali unaonesha dhamira ya kujenga mfumo shirikishi wa huduma za afya.
Kwa kuhitimisha, Prof. Masenga aliwahimiza washiriki kutumia vyema fursa hiyo kwa kushiriki kikamilifu, kuuliza maswali na kujenga mahusiano ya kitaaluma yatakayodumu kwa muda mrefu akiamini kuwa maarifa yatakayopatikana katika siku hizi mbili yataenda kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za radiolojia na afya kwa ujumla.
Related Stories